Matendo
Chapter 4
Biblia Takatifu (Swahili…

Read in

Smith–Van Dyck Arabic Bible (فان دايك)Judson Burmese Bible (1840)Chamorro: Gospels, Acts and PsalmsChinese Union Version, punctuated (Simplified)Chinese Union Version, punctuated (Traditional)Coptic New TestamentCoptic New Testament (Bohairic)Kralice Bible (1613)Testamenta Marra (Dieri New Testament)Petrus Canisius Bible, 1939 (De Heilige Schrift)Asang Khongca Bible (Eastern Khumi Chin, 2019)Berean Standard BibleDouay-Rheims Bible, American Edition (1899)King James Version with ApocryphaWorld English BibleLondona Biblio (Esperanto, 1910)Louis Segond 1910Lutherbibel 1912Greek New Testament, word by word (STEPBible TAGNT)Greek New Testament: 1904 Patriarchal Text (Byzantine)Greek New Testament: Byzantine Text (Robinson–Pierpont 2018)Greek New Testament: Textus ReceptusSBL Greek New TestamentBaibala Hemolele (Hawaiian Bible, 1868 revision)Modern Hebrew BibleDiodati Bibbia 1885Freedom Bible (フリーダム・バイブル)Korean Bible, 1910 (한국어 성경)Bible Mutal (Kosraean)Clementine Vulgate, 1598Baibal Olcim (Matupi Chin)Old Persian Version (ترجمه قدیم)Kadede Kap (Pohnpeian New Testament and Psalms)Bíblia Portuguesa Mundial (Brazilian Portuguese)Cornilescu Bible (1924), Cyrillic scriptSynodal Translation (Синодальный перевод)Daničić–Karadžić Bible (1868), CyrillicReina-Valera 1909Biblia Takatifu (Swahili): New Testament portionsFreedom Bible (Thai)Tongan Bible, Revised West VersionKulish and Puluj Bible (1905)Vietnamese Bible (1923 translation)
Compare
Aa
Text size
Line width
Verse numbers

1Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa Hekalu pamoja na Masadukayo walifika.

2Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonyesha wazi kwamba wafu watafufuka.

3Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake.

4Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu elfu tano.

5Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na walimu wa Sheria, walikusanyika pamoja huko Yerusalemu.

6Walikutana pamoja na Anasi, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa Kuhani Mkuu.

7Waliwasimamisha mitume mbele yao, wakawauliza, “Ninyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?”

8Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, “Viongozi na wazee wa watu!

9Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima,

10basi, ninyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye ninyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka wafu.

11Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema: Jiwe mlilokataa ninyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.

12Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye.”

13Hao wazee wa baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu.

14Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu.

15Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha.

16Wakaulizana, “Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba mwujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo.

17Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu.”

18Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu.

19Lakini Petro na Yohane wakawajibu, “Amueni ninyi wenyewe kama ni haki mbele ya Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii yeye.

20Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia.”

21Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo.

22Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arobaini.

23Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee.

24Waliposikia habari hiyo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, “Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo!

25Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, babu yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: Kwa nini mataifa yameghadhibika? Mbona watu wamefanya mipango ya bure?

26Wafalme wa dunia walijiweka tayari, na watawala walikutana pamoja, ili kumwasi Bwana na Kristo wake.

27“Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye umemtia mafuta.

28Naam, walikutana ili wafanye yale ambayo ulikusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako.

29Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari.

30Nyosha mkono wako uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu.”

31Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila uoga.

32Jumuiya yote ya waumini ilikuwa moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo.

33Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi.

34Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza

35na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake.

36Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita jina Barnaba (maana yake, “Mtu mwenye kutia moyo”).

37Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume.

Tip: use the ← and → keys to turn chapters.