Matendo
Chapter 3
Biblia Takatifu (Swahili…

Read in

Smith–Van Dyck Arabic Bible (فان دايك)Judson Burmese Bible (1840)Chamorro: Gospels, Acts and PsalmsChinese Union Version, punctuated (Simplified)Chinese Union Version, punctuated (Traditional)Coptic New TestamentCoptic New Testament (Bohairic)Kralice Bible (1613)Testamenta Marra (Dieri New Testament)Petrus Canisius Bible, 1939 (De Heilige Schrift)Asang Khongca Bible (Eastern Khumi Chin, 2019)Berean Standard BibleDouay-Rheims Bible, American Edition (1899)King James Version with ApocryphaWorld English BibleLondona Biblio (Esperanto, 1910)Louis Segond 1910Lutherbibel 1912Greek New Testament, word by word (STEPBible TAGNT)Greek New Testament: 1904 Patriarchal Text (Byzantine)Greek New Testament: Byzantine Text (Robinson–Pierpont 2018)Greek New Testament: Textus ReceptusSBL Greek New TestamentBaibala Hemolele (Hawaiian Bible, 1868 revision)Modern Hebrew BibleDiodati Bibbia 1885Freedom Bible (フリーダム・バイブル)Korean Bible, 1910 (한국어 성경)Bible Mutal (Kosraean)Clementine Vulgate, 1598Baibal Olcim (Matupi Chin)Old Persian Version (ترجمه قدیم)Kadede Kap (Pohnpeian New Testament and Psalms)Bíblia Portuguesa Mundial (Brazilian Portuguese)Cornilescu Bible (1924), Cyrillic scriptSynodal Translation (Синодальный перевод)Daničić–Karadžić Bible (1868), CyrillicReina-Valera 1909Biblia Takatifu (Swahili): New Testament portionsFreedom Bible (Thai)Tongan Bible, Revised West VersionKulish and Puluj Bible (1905)Vietnamese Bible (1923 translation)
Compare
Aa
Text size
Line width
Verse numbers

1Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wanakwenda Hekaluni, wakati wa sala.

2Na pale karibu na mlango wa Hekalu uitwao “Mlango Mzuri”, palikuwa na mtu mmoja, kiwete tangu kuzaliwa. Watu walimbeba huyo mtu kila siku na kumweka hapo ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia Hekaluni.

3Alipowaona Petro na Yohane wakiingia Hekaluni, aliwaomba wampe chochote.

4Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia, “Tutazame!”

5Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.

6Kisha Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!”

7Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu.

8Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao Hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu.

9Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu.

10Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule “Mlango Mzuri” wa Hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata.

11Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa “Ukumbi wa Solomoni,” ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane.

12Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, “Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea?

13Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Yesu mtumishi wake. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru.

14Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini ninyi mlimkataa, mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe.

15Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uzima. Lakini Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo.

16Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa nguvu mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya kabisa mtu huyu kama mnavyoona nyote.

17“Sasa ndugu zangu, nafahamu kwamba ninyi na wakuu wenu mlitenda hayo kwa sababu ya kutojua kwenu.

18Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza zamani kwa njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke.

19Basi, tubuni mkamrudie Mungu ili afute dhambi zenu.

20Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika rohoni na kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu.

21Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika wakati wa kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii wake watakatifu wa tangu zamani.

22Kwa maana Mose alisema, Bwana Mungu wenu atawapelekeeni nabii kama mimi kutoka kati yenu ninyi wenyewe.

23Yeyote yule ambaye hatamsikiliza nabii huyo atatengwa mbali na watu wa Mungu na kuangamizwa.

24Manabii wote, kuanzia Samweli na wale waliomfuata, walitangaza habari za mambo haya ambayo yamekuwa yakitendeka siku hizi.

25Ahadi zile Mungu alizotoa kwa njia ya manabii ni kwa ajili yenu; na mnashiriki lile agano Mungu alilofanya na babu zenu, kama alivyomwambia Abrahamu: Kwa njia ya wazawa wako, jamaa zote za dunia zitabarikiwa.

26Basi, ilikuwa kwa ajili yenu kwanza kwamba Mungu alimfufua mtumishi wake, alimtuma awabariki kwa kumfanya kila mmoja wenu aachane kabisa na maovu yake.”

Tip: use the ← and → keys to turn chapters.